Mcheza sinema maarufu wa Kimarekani, Angelina Jolie, ametangaza kwamba
amefanyiwa operesheni ya kuondosha matiti yake yote mawili ili kupunguza
uwezekano wa kupata saratani ya maziwa na ya kizazi.
Kwa mujibu wa makala yake iliyochapishwa leo kwenye gazeti la The New York Times
na kupewa jina "Chaguo langu la kitabibu", Angelina Jolie amesema
ameamua kutangaza jambo hilo hadharani ili kuwapa moyo wanawake wengine
wenye historia ya familia zinazouguwa saratani.
Mama yake mwenyewe Angelina alifariki akiwa na miaka 56 kutokana na
maradhi hayo. Sasa muigizaji huyo maarufu wa sinema duniani, anasema
anawataka wanawake wenye hali kama yake kutafuta ushauri wa kitabibu na
kufanya uamuzi baada ya kuwa na taarifa za kutosha ili waweze kuendelea
kufanya kazi, kama alivyofanya yeye.
"Licha ya kuweza kulifanikisha hili na kubakia kimya kwa muda mrefu,
sasa naandika kulitangaza kwa sababu natarajia kuwa wanawake wengine
wanaweza kufaidika na uzoefu wangu." Ameandika mjumbe huyo maalum wa
Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya wakimbizi.
Uamuzi mgumu lakini muhimu
Jolie aliamua kufikia uamuzi huo wa kuyaondosha matiti yake yote
mawili, kwa sababu alifahamishwa na madaktari wake kwamba alikuwa na
chembechembe inayoongeza hatari ya kupata saratani kwenye maziwa yote
mawili na kwenye fuko lake la uzazi.
Kutokana na chembechembe hiyo iitwayo BRCA1, madaktari walikisia kwamba
alikuwa kwenye kiwango cha asilimia 87 ya hatari ya kupata saratani ya
maziwa na asilmia 50 ya kupata saratani ya kizazi.
"Baada tu kujua kwamba huo ndio ukweli kuhusu hali yangu, niliamua
kuchukua hatua za kabla na angalau kupunguza kiwango hicho cha hatari
kadiri nilivyoweza. Nikafanya uamuzi wa kuondosha matiti yangu yote
mawili. Nilianza na maziwa kwa kuwa saratani ya maziwa ni kubwa zaidi
kuliko hatari ya ile ya fuko la uzazi, na operesheni ya fuko la uzazi ni
kubwa zaidi," ameandika Jolie.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 37 amesema kwamba tarehe 27 Aprili
alikamilisha miezi mitatu ya taratibu za kitabibu kuhusiana na
operesheni hiyo ya kuondosha matiti na kwamba sasa kiwango cha uwezekano
wa kupata saratani kimepungua hadi asilimia tano.
Jolie na mumewe, ambaye pia ni muigizaji maarufu, Brad Pitt, wana watoto
watatu wa kuwazaa na watatu wa kuwalea, na ameandika kwamba sasa
anaweza kuwaambia watoto wake kwamba hawapaswi kuwa na hofu ya kumpoteza
mama yao kwa sababu ya saratani.
No comments:
Post a Comment