Tuesday, July 2, 2013

GEORGE BUSH NA OBAMA WATAKUTANA ANA KWA ANA KATIKA ARDHI YA TANZANIA LEO


Rais wa Marekani, Barack Obama na mtangulizi wake, George W. Bush, leo wanakutana ana kwa ana kwenye ardhi ya Tanzania watakapoweka mashada kwenye Ubalozi wa zamani wa Marekani uliolipuliwa mwaka 1998.


Rais Obama ameweka rekodi ya kuwa mtu wa kwanza mweusi kuchaguliwa kuongoza Marekani, akipokea wadhifa huo kutoka kwa Rais Bush, ambaye aliiongoza taifa hilo kuanzia mwaka 2000-2008.


Kitendo cha vigogo hao kukutana nchini ni cha
kihistoria na kinadhihirisha jinsi Marekani ilivyoipa kipaumbele Tanzania kwa masuala ya diplomasia.

Viongozi hao wawili, wapo Tanzania wakati Rais Obama akimalizia ziara yake ya Afrika na Bush atakuwa na mkewe, Laura, watahudhuria mkutano wa wake za marais wa Afrika unaodhaminiwa na Taasisi ya Bush Foundation.

Pia, Michelle Obama, atahudhuria mkutano huo kabla ya kuondoka kurejea Marekani.

Balozi mbili za Marekani za Dar es Salaam na Nairobi, Kenya zilishambuliwa kwa wakati mmoja Agosti 7, 1998.

Obama ataweka shada kama sehemu ya kumbukumbu ya tukio hilo na Bush ataungana naye katika shughuli hiyo.
Hata hivyo, viongozi hao hawatahutubia wakati wa shughuli hiyo.


Rais Obama ametoa pongezi kwa sera za Bush Afrika hasa kwa kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi.


Hata hivyo, utawala wa Rais Obama umejikita zaidi katika mapambano dhidi ya ugaidi.


Kuna kamandi ya Jeshi ya Africom, ambayo ina kazi kubwa ya kukabiliana na ugaidi barani humu.


Operesheni kubwa za Africom zipo nchi za Afrika Kaskazini, Somalia na Afrika ya Kati ambako wanamsaka kiongozi wa Kundi la Waasi la Lord Resistance, Joseph Kony.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment