Wednesday, June 26, 2013

CHADEMA WAKATAZWA KUVAA KOMBAT BUNGENI...!!

Kombati za CHADEMA mzozo
Siku moja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na wabunge wenzake watatu kuzuiwa kuingia bungeni juzi, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa kombati zao zinakiuka kanuni.

Mbowe na wabunge wenzake wa CHADEMA, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa na askari kwa madai kuwa wamevalia sare za chama ambazo kikanuni haziruhusiwi.

 
 Uamuzi huo uliibua hali ya sintofahamu kwa wabunge wa CHADEMA kutokana na Mbowe kuvalia vazi hilo mara nyingi tangu aingie bungeni mwaka 2010.

Licha ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la ‘safari suti’ kwa wanaume lenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa uamuzi huo unaacha maswali mengi yanayohitaji majibu.

Akizungumzia uamuzi huo jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema suti hizo za wabunge wa CHADEMA zilikiuka kanuni ya 149 (3) (b) (i).

Kipengele hicho cha kanuni kinasomeka kuwa inaruhusiwa suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia.

Joel alifafanua kuwa yawezekana huko nyuma wamekuwa wakifanya makosa kwa kuwaruhusu wabunge hao kuingia na suti hizo, lakini sasa kuanzia juzi wameamua kuanza
 kuchukua hatua ya kuwazuia.

“Zile wanasema sio sare ya chama, lakini wote tunawaona kwenye mikutano na shughuli za chama ndizo zinavaliwa na isitoshe tuliwahi kuwatahadharisha kuwa ziko kinyume na kanuni wasizivalie bungeni ila wamekuwa wakiendelea kuzivaa,” alisema.

Licha ya kanuni hiyo kuwa kimya kuhusu kuvaa sare za vyama bungeni, Joel alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa ni busara ya spika wa wakati huo, Samuel Sitta, lakini haujaingizwa kwenye kanuni kimaandishi.

Tanzania Daima Jumatano lilitaka kufahamu ni kwanini uamuzi huo ukaanza ghafla juzi baada ya wabunge wa CHADEMA kurejea kutoka jijini Arusha, na Joel bila kufafanua alisema: “Kawaulize walipanga nini wakiwa Arusha? Ndiyo maana tukaamua kuchukua hatua.

“Bora tukaonekana tumewaonea kuliko kuendelea kufumbia macho kanuni. Tuwe wawazi kombati zao zina nakshi kupitiliza kwa mujibu wa kanuni. Kwanini wakina Halima Mdee na Vicent Nyerere tuliwaacha wakaingia? Mbona kombati za Zitto zinatofautiana na wengine?”
Alipotakiwa kufafanua kama kweli walishaonywa wasivae kombati hizo bungeni,

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika alisema Joel hajui kanuni za Bunge ndiyo maana amekuwa anampotosha spika na viongozi wa Bunge kufanya uamuzi wa ajabu.

“Wametuzuia juzi kwa sababu ya maelezo ya akina Pinda na Serikali ya CCM, sio kwa sababu ya ukiukwaji wa kanuni za Bunge. Kumekuwa na utamaduni wa hovyo wa kutafsiri vibaya kanuni za Bunge kwa lengo moja tu, kuwadhibiti CHADEMA,” alisema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alitolea mfano akisema kuwa walizuiliwa kuingia ukumbini na askari polisi wasiokuwa na mamlaka ya kuwazuia kuingia ndani bali walitakiwa wasubiri amri ya spika kuwatoa ukumbini ndipo wawatoe.

“Hayo yote hawezi Joel kufahamu, anafanyia uzoefu alioupata wakati anafanya kazi Makao Makuu ya CCM wakati wa Bunge la chama kimoja,” alisema Mnyika.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa walishangazwa na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa miaka yote na kuingia nayo bungeni.

Lissu alisema kuwa hatua hiyo waliichukulia kama mkakati maalumu wa Serikali ya CCM kutaka kuwazima kabisa kuhakikisha hawapati nafasi ya kuingia bungeni ili kujibu tuhuma walizosingiziwa kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini Arusha.

“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume na utaratibu wa kanuni askari wa kawaida wameingizwa hadi bungeni,” alisema.

Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama chake isipokuwa kanuni zimeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume.

Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(b) kwa wanaume wanaruhusiwa kuvaa (i) suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia;

(ii) vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu; (iii) suti kamili ya kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; (iv) koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v) tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.


No comments:

Post a Comment