Dar es Salaam. Makachero wa Marekani
wameendelea na matayarisho ya mwisho ya ziara ya Rais Barack Obama,
ambapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere walikuwa na
kazi ya kuunganisha helikopta za doria.
Makachero hao walikuwa wakiunganisha
helikopta sita zilizosafirishwa vipande vipande kutoka Marekani, ambapo
meli mbili za kivita na ndege moja pia zimewasili.
Rais Obama tayari yuko katika ardhi
ya Afrika, ambapo leo anatarajiwa kwenda Afrika Kusini baada ya kumaliza
ziara yake ya kwanza Senegal na anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa
jana na Mwananchi unaonyesha Marekani imeleta helikopta hizo kwa ajili
ya ulinzi wa Rais Obama, zikiwemo meli zilizobeba helikopta nyingine
mbili na ndege.
Habari zilizopatikana kutoka kwa
wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,zinasema
kuwa helikopta sita zinaunganishwa katika sehemu ya karakana ya Kikosi
cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mpashaji mmoja aliliambia gazeti hili
kuwa helikopta hizo zililetwa kama vipande vipande vilivyosafirishwa
kama mzigo kwenye meli za kivita zilizotia nanga jijini Dar es Salaam.
“Nilikaribia kwenye eneo la karakana
na nikashangaa kuona jinsi jamaa walivyokuwa ‘bize’ wakiunganisha vyuma
mbalimbali na kutengeneza helikopta hizo,” aliongeza mpashaji wetu,
ambaye alibahatika kusogelea eneo hilo licha ya kuwepo kwa ulinzi mkali.
Inaaminika kuwa helikopta hizo
zitakuwa zinasaidia kusafirisha watu na mizigo kutoka kwenye meli za
kivita ambazo zimeegeshwa kwenye Kikosi cha Maji cha JWTZ.
Pia helikopta mbili zinaaminika ziko katika meli ambazo zimeegeshwa huko Kigamboni.
Meli za kivita na ndege ya kijeshi
Katika hatua nyingine, meli mbili za kivita ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu zimeegeshwa Kigamboni.
“Jamaa wana meli kali kwa kweli, mimi
nimekuwa askari wa Kikosi cha Maji kwa muda mrefu na kufanya mazoezi na
mataifa kadhaa, lakini sijaona meli kama zile.
“Wamarekani wanatisha sana. Meli zao
zina zana muhimu za kivita. Pia wanafuatilia kila kitu kinachoweza
kuhatarisha usalama wao. Hawaamini mtu kabisa wala kudharau chochote,”
aliongeza mtoa habari mmoja.
Ndege ya kijeshi
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna ndege ya Jeshi la Marekani lakini imeegeshwa kwenye karakana ya Kikosi cha Anga cha JWTZ.
Ndege hiyo inadaiwa iko nchini tangu
mwanzoni mwa wiki hii, ingawa kuna taarifa kuwa zipo ndege nyingine
ambazo zimekuwa zikitua na kuruka.
“Ndege nyingi za Wamarekani zinatua
nchini kwa kipindi cha wiki mbili sasa, zaidi zinaleta watu, ambao
nahisi ni wale wanaohusika na usalama na mizigo.
“Kimsingi kuna mambo mengi
yanaendelea hapa uwanja wa ndege. Ila msisahau pia kuna ujio wa marais
kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya mkutano wa Smart
Partnership ndiyo maana kuna mengi yanaendelea hapa,” kiliongeza chanzo
chetu.
Matapeli waibuka
Kuna habari pia, kuna kundi la watu
limeibuka jijini Dar es Salaam ambalo linataka kutapeli wakazi wa jiji
kwa kutumia mgongo wa ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama.
Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu,
Suleiman Kova aliliambia gazeti hili kuwa wamepelekewa kesi tatu za
majaribio ya watu kupora wengine kwa kutumia mgongo wa Obama.
Ziara ya Rais Obama imesababisha
kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri na malazi, hali iliyosababisha
kuibuka kwa matapeli wanaowalenga watu wenye magari yenye hadhi kwa
wageni wa nje.
Pia hali hiyo imechangiwa zaidi
kutokana na ugeni wa viongozi wapatao 11 kutoka mataifa mbalimbali
duniani, wanaohudhuria mkutano wa Smart Partnership unaoanza leo jijini
Dar es Salaam.
Kova alisema kundi hilo limekuwa likiwasiliana na watu wanaomiliki magari ya kifahari ili wakodishe magari yao.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment